Wednesday, March 27, 2013

Mafunzo ya JKT yazinduliwa rasmi na Mheshimiwa Raisi Kikwete


Pwani na Handeni.  Amiri Jeshi Rais Jakaya Kikwete, amezindua rasmi mafunzo ya miezi mitatu ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa  vijana  wa mujibu wa sheria na vijana.
Jumla ya vijana 1,222 wanashiriki mafunzo hayo.
Rais Kikwete ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, pia   amefunga rasmi mafunzo maalumu ya JKT yaliyowashirikisha wabunge 47.
Mafunzo hayo ya awali, yalidumu kwa wiki tatu na yalifanyika katika vikosi mbalimbali nchini.
Hata hivyo, ni wabunge 23 tu waliofanikiwa kuhitimu mafunzo hayo jana.
Rais aliwasili katika Viwanja vya Ruvu JKT kwa helikopta na kisha kupewa taarifa ya jeshi hilo na baadaye kuzindua mafunzo ambayo alisema ni kwa nchi nzima na yatahusisha vijana 4,710 wa mujibu  wa sheria.
Alisema vijana wengine 6,722 watakuwa ni wa kujitoleana kwamba tayari wameshatawanywa katika vikosini. Rais Kikwete alisema uzinduzi huo ni wa kihistoria kwa sababu  mafunzo ya JKT ndiyo sasa yanaanza tena baada ya kufutwa kwa zaidi ya miaka 20 iliyopita kutokana na kuyumba kwa uchumi.
Alisema hata hivyo  kutokana na umuhimu, Serikali sasa imeamua kurudisha mafunzo hayo ingawa bado kuna  changamoto ya fedha.
Kwa mujibu wa Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, ni kiasi cha Sh7.5 bilioni  tu ndizo zilizotengwa kwa shughuli hizo.
Mkuu wa JKT, Meja Jenerali Raphael Muhuga alisema mafunzo hayo  yatafanyika kwa miezi mitatu na baada ya muda huo vijana wengine watachukua nafasi.
Alisema utaratibu wa vijana kujiunga na jeshi, utakuwa unafanyika kabla ya vijana kwenda vyuo vikuu.
Katika risala yao wahitimu tisa wa Kikosi cha Ruvu JKT, waliishauri Serikali kuboresha masilahi ya askari.
Wabunge hao ni Ester Bulaya, Halima Mdee, Neema Hamid, David Silinde, Murtaza Mangungu, Livingston Lusinde, Yusuph Khamis, Said Mtanda na Mendrad Kigola
                                   
.

0 comments:

Post a Comment